 |
Arsene Wenger |
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini kufungwa kwa Ufaransa au England kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi D utaozikutanisha timu hizo utapoteza matumani yao Euro 2012.
England itavaa Ufaransa mjini Donetsk hapo Jumatatu mechi ambayo Wenger anaamini itaamua hatma ya kundi hilo lililokuwa na nyingine Sweden na wenyeji wenza Ukraine.
Wenger alisema hayo wakati wa mahojiano na tovuti ya Arsenal (www.arsenal.com) kuwa England wana kibarua kigumu zaidi baada ya kuwakosa nyota wake kadhaa wakiwemo Wayne Rooney ambaye amefungiwa kucheza mechi mbili za kwanza za nchi hiyo.
"Mechi ya ufunguzi kati ya England na Ufaransa na kukosekana kwa Rooney, unaweza kusema ni mchezo ambao hatakiwi kupoteza," alisema Wenger.
"Kwanini? Kwa sababu hutaweza kurudi kwenye mstari wa ushindani kutokana na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa nchi zao wanaotaka kuona timu yao ikishinda tu.
"Mechi hiyo itaamua hatma ya kundi lote. Kama ikimalizika kwa sare 0-0, hapo kundi litakuwa wazi kwa wote, lakini kama moja atafungwa atakuwa wamejifungulia njia ya kutolewa kwa sababu Ukraine itaifunga moja ya nchi hizo mbili na Sweden ni timu ngumu kufungika."
Wenger anaamini mchezo wa kwanza wa England ndiyo utakaoamua hatma yao wakiwa na kocha wao mpya Roy Hodgson.
"England watamkosa Rooney, wana kocha mpya na hawajakaa pamoja... ni vigumu kuwategeneza na kuwa timu kwa haraka," alisema.
"Unaweza kufanikiwa au hapana? Hiyo itajulikana baada ya mechi ya kwanza.
"Faida pekee kwa England ni kuwa na kocha mzoefu Hodgson aliyewahi kufundisha timu ya taifa na mwenye uzoefu na mashindano haya na mwenye kuwafahamu vizuri wachezaji wa England.
"Kwa sasa England bado wanaangaika kujenga kujiamini na kama wakifanikiwa kufanya hilo, basi wataweza kupata matokeo mazuri."
Wakati huohuo; Wenger anaamini Ufaransa ina uwezo wa kurudia mafanikio yake ya Euro 2000, lakini kama wachezaji wake wakiweka kado mawazo mabaya yaliyowakutaka kwenye fainali za Kombe la Dunia 2010.
"Wachezaji wa Ufaransa wanaweza kutwaa ubingwa wa fainali hizi," alisema Wenger.
"Lakini bado hawajiamini vya kutosha kwa sababu ya tukio lililowakuta Afrika Kusini.
Mategemeo kwa Ufaransa ni madogo kwa sababu ya jambo hilo, lakini wana uwezo.
"Wana wachezaji nyota kama Benzema, (Franck) Ribery, (Samir) Nasri. Kama wakiandaliwa vizuri kisaikolojia naweza kuwashangaza wengi kwenye michuano hiyo."