
Hii ni kwa shabiki wa Arsenal. Hebu kaa kimya, kwa sekunde
chache tu, kisha jiulize. Ingekuwa vipi Luis Suarez angekuwa Arsenal kwa
sasa? Ungetaka abaki, au aende zake huko anakohitajika? Usijibu.
Mengi yanasemwa katika kipindi hiki, hasa baada ya
Arsenal kupeleka ofa ya pauni 40,000,001 Liverpool, wakimtaka straika
huyo, Suarez. Hakuna shaka, shabiki yeyote wa Arsenal ni mtu mwenye
furaha kubwa kwa sasa kwasababu klabu yao inafukuzia usajili wa moja ya
wanasoka wenye vipaji kwenye soka la kisasa.
Na zaidi ya hilo, Suarez amekuwa fundi mzuri wa
kufunga mabao. Anafanya hivyo kila anapocheza. Lakini, linapokuja suala
la kutaka kumsajili, Arsenal pamoja na furaha yao yote, inapaswa
kujiuliza maswali ya msingi. Anafaa au usajili wake unataka kufanywa kwa
kujikosha tu kwa watu kuwa nao wanasajili wachezaji wenye majina?
Ingekuwa vipi, Suarez kwa sasa angekuwa mchezaji
wa Arsenal na analazimika kuhama? Tena angekuwa analazimisha kuhamia kwa
timu kama Manchester City? Msimu uliopita, Robin van Persie alihamia
Manchester. Mashabiki wengi sana wa Arsenal walikasirishwa na hilo, kwa
sababu moja tu. Walimvumilia wakati wa majeruhi, walimsapoti kwa kila
kitu na kisha akawaacha na kwenda kwa wapinzani, Manchester United.
Haikuwa vizuri kwa mashabiki wa Arsenal kwa uamua wa kuhamia Manchester
United.
Na mbaya zaidi alifanya hivyo baada ya msimu mmoja kucheza kwa
kiwango kikubwa, bila ya kusumbuliwa na majeruhi yoyote. Hili halina
tofauti sana na hadithi ya Suarez. Misimu miwili iliyopita, Suarez
amekuwa mtuhumiwa wa matukio ya utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja,
lakini bado klabu yake ilimsapoti kwa kila hali. Baada ya kuandamwa na
vyombo vya habari, straika huyo aliibuka na wazo la kutaka kuhamia
ng’ambo ya nchi.
Lakini, baadaye akadai kwamba anataka kujiunga na
timu itakayompa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kujali
kama itakuwa ndani ya England au la. Kesi ya Suarez ipo tofauti na ya
Van Persie, mshambuliaji huyo wa Uruguay ni mbinafsi, anajifikiria yeye
zaidi. Kwa tabia yake hiyo, Arsenal wanapaswa kujiuliza kabla hawajatoa
pesa yao nyingi kumsajili.
Arsene Wenger hapaswi kusahau kwamba ni Real
Madrid, ambayo ni chaguo la kwanza la Suarez. Si Arsenal. Pia fikiria
hili, Suarez ametua Arsenal, akaisaidia kutwaa taji la Ligi Kuu na kisha
akafunga mabao 30. Unadhani kuna uhakika atabaki Arsenal mchezaji huyu?
Mchezaji ambaye mapenzi yake ya kwanza yapo kwingine? Anadhani
atazikataa Real Madrid na Barcelona zitakapokuja na ofa zao kutaka
kumsajili?
Suarez ni mchezaji mahiri kweli, hilo halina
pingamizi. Lakini, kwanini Wenger hakumsajili mchezaji huyo wakati
alipokuwa Ajax. Kwa shabiki wa Liverpool uhamisho wake utamfanya kuwa na
hasira, kwa sababu anahama baada ya kupata sapoti kubwa ya matatizo
yake yenye utata. Kwa upande wa Arsenal, ukiweka ushabiki pembeni,
kumsajili Suarez ni kujiweka katika hali ya hatari. Ikumbukwe, atahamia
hapo akiwa na adhabu ya kukosa mechi sita. Je, kuna uhakika kwamba
amepona ugonjwa wake na hatamng’ata mchezaji mwingine atakapokuwa ndani
ya jezi za Arsenal?
Je, hatakumbana na adhabu ndefu wakati atakapotua
Emirates? Je, hataamsha tena sakata la kutaka kuhama baada ya misimu
miwili hasa ukizingatia mapenzi yake si kuichezea Arsenal? Kwa Suarez,
Arsenal inajitengenezea bomu, itamsajili kwa pesa nyingi na kisha baada ya
miaka miwili ataomba kwenda Barcelona au Real Madrid. Sawa, humtarajii
Suarez azekee Emirates, lakini itakuwa hasara kama ataomba kuondoka
baada ya misimu miwili.
Huu ndio wasiwasi wa kuwa na mchezaji kama
Suarez, ana uwezo lakini hakupi uhakika wa kuwa na mipango ya kujenga
timu kupitia yeye. Real Madrid na Barcelona bado zitaendelea na
chokochoko zao za kumsajili kama ataendeleza makali yake atakapotua
Emirates.
Kwa kiwango cha Suarez, kama hajapata tatizo la
majeraha, suala la kung’ara hilo halina mjadala. Unatarajia kuliona
kutoka kwake. Hakuna ubishi Arsenal itakuwa imepiga bao watakapoinasa
huduma yake, lakini tatizo lake ni moja tu. Haaminiki, hakawii kuchafua
hali ya hewa. Hili ndilo lililopo upande wa pili wa sarafu katika
usajili wa Suarez Arsenal.
source: mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment