SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF), limempa kocha wa timu za vijana za Tanzania, Kim Poulsen, jukumu jipya la kuinoa timu ya wakubwa, Taifa Stars na kumpiga chini kocha wa sasa, Jan Poulsen.
Kim, ambaye yupo na Ngorongoro nchini Sudan atarudi Jumatatu na kutangaza kikosi cha Taifa Stars kujiandaa kwa mchezo dhidi ya Ivory Coast, Juni Mosi.
Jan amekamilisha mkataba wake mwisho wa mwezi uliopita na mpaka sasa hakuna mazungumzo yoyote ya kuongeza muda yaliyofanyika.
Duru za ndani ya TFF zimethibitisha kwamba hatakiwi tena na Kim amepewa jukumu hilo la kuongoza Taifa Stars.
Hiyo inamaanisha kwamba Kim aliyeletwa nchini kwa mapendekezo ya Jan, sasa yupo na Ngorongoro Heroes nchini Sudan lakini Juni Mosi ataiongoza Stars nchini Ivory Coast kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia na baadaye dhidi ya Gambia Juni 6.
Baada ya hapo ataiongoza Stars pia kwenye mechi dhidi ya Msumbiji ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani.
Kim ameshaambiwa suala hilo na tayari ameanza kufuatilia mechi mbalimbali za Ligi Kuu mikoani Dar es Salaam kutengeneza kikosi chake kipya ambacho watu wake wa karibu wanadai kitakuwa na vijana wengi tofauti na Stars ya sasa.
Jan amekuwa kwenye wakati mgumu katika siku za karibuni kutokana na kuyumba kwa timu hiyo kwenye michuano mikubwa huku akiwaacha mastraika, Danny Mrwanda wa klabu ya DT Long ya Vietnam na Mbwana Samatta wa TP Mazembe kwa madai kuwa hawajitumi.
Kuwaondoa wachezaji hao kikosini kumemweka kwenye wakati mgumu kwa vile walioziba nafasi zao wameshindwa kuonyesha jipya walilonalo.
TFF ilimtaka Jan kutangaza kikosi cha Taifa Stars jana Ijumaa, lakini aligoma kwa madai kuwa yeye si kocha wa timu hiyo na kesho Jumapili anakwenda Nigeria katika kazi zake za ukufunzi.
No comments:
Post a Comment